HUDUMA za kujifungua kwa wajawazito katika zahanati ya Kata ya
Iglansoni, wilayani Ikungi, Singida zimesimama kwa muda usiojulikana
kutokana na chumba kilichokuwa kikitumika kwa shughuli hizo
kubadilishwa matumizi.
Chumba hicho sasa kimekuwa nyumba ya kuishi muuguzi mkunga wa zahanati hiyo.
Hatua hiyo imefikiwa na uongozi wa kata hiyo baada ya muuguzi mkunga
huyo, Meriani Misai kutokuwa na nyumba ya kuishi baada ya dari la
nyumba aliyokuwa akiishi kuanguka na popo kugeuza makazi yao kwa
kipindi kirefu sasa.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Iglansoni, Rehema Majii alieleza muuguzi
huyo alikuwa akikosa usingizi, hasa wakati mvua zinapoanza kunyesha na
hivyo kumfanya kukaa kwenye kiti bila kulala kutokana na nyumba kuvuja.
“Kwa kweli nyumba ya nesi haifai inavuja, kwani mpaka ikafikia siku
moja akashinda akiwa amekaa kwenye kiti bila kulala na mvua ikiwa
inanyesha…kwa hiyo ilibidi tufanye utaratibu, tumemhamishia zahanati,”
alifafanua Majii.
Kwa mujibu wa ofisa mtendaji huyo, kutokana na mtumishi huyo kuhamia
kwenye chumba kinachotegemewa kutoa huduma za wajawazito, huduma za
aina hiyo zimekuwa hazitolewi kama ilivyokuwa awali.
“Kwahiyo kwa sasa hata zile shughuli za kuhudumia wagonjwa zimekuwa
hazitolewi kama zinavyostahili kutokana na mhudumu huyo kuhamia kwenye
zahanati hiyo,” alisisitiza ofisa mtendaji huyo.
Kwa upande wake, muuguzi mkunga, Misai, alisema alikuwa akiteseka
kwa kuwa nyumba aliyokuwa akiishi ni mbovu, popo wamegeuza makazi kwa
kipindi cha miaka mitatu sasa licha ya kutoa taarifa kwa wakuu wa idara
wilayani.
Kwa mujibu wa Misai, wajawazito wanalazimika kutembea umbali wa zaidi
ya kilomita 50 kufuata huduma hizo katika zahanati ya Kata ya
Muhintiri au mbele zaidi kwenye makao makuu ya Tarafa ya Ihanja.
Akizungumzia malalamiko ya mtumishi huyo, Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Magayane Protace, licha ya kukiri
jitihada zinazofanywa na idara ya afya, lakini hakusita kutoa suluhisho
la awali la mtumishi aliyekuwa akiishi ndani ya nyumba hiyo.
Alisema wameamua kumsaidia muuguzi mkunga huyo wakati idara
inaendelea na jitihada za kulitatua tatizo hilo, alimuagiza Ofisa
Mtendaaji wa kata hiyo, Majii, kumtafutia mara moja nyumba ya kupanga
na kwamba halmashauri itamlipia gharama za pango kwa kipindi cha miezi
mitatu.
Kaimu Mganga mkuu wa wilaya ya Ikungi, Dk. Henry Mbando alisema
kutokana na dharura hiyo wameshafanya tathimini ya zaidi ya sh milioni
sita za CHF kwa ajili ya kuifanyia ukarabati nyumba hiyo.
Chanzo;Tanzania daima
0 comments:
Post a Comment